Skip to main content
BUNGE LA TAIFA KUTUMIA KISWAHILI KATIKA MIJADALA BUNGENI

BUNGE LA TAIFA KUTUMIA KISWAHILI KATIKA MIJADALA BUNGENI

Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Bunge la Taifa la Kenya imekuwa safari ya mwendo wa kobe.

Mara ya kwanza kwa Bunge hili kukumbatia matumizi ya Kiswahili ilikuwa mnamo mwaka wa 1974. Hii ni baada ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta kutangaza kuwa Kiswahili iwe mojawapo ya lugha za kutumiwa kuendesha mijadala Bungeni.  Alitoa amri hiyo baada ya Kiswahili kupandishwa hadhi na kuwa lugha ya Taifa nchini Kenya, kulingana na chapisho la Lyndon Harries.

Hivyo basi, uzinduzi wa machapisho ya Kiswahili na Kiswahili- Kiingereza ya Kanuni za Kudumu za Bunge la Taifa ni hatua ya pili muhimu katika maendeleo ya matumizi ya lugha hii katika shughuli za asasi hii, baada ya hatua ya Rais wa kwanza wa Jamhuri mnamo mwaka wa 1974.

Hafla ya Uzinduzi huo iliongozwa na Rais Uhuru Kenyatta mda mfupi baada ya kutoa Hotuba yake katika kikao cha Pamoja cha Bunge la Kitaifa na Seneti, mnamo Novemba 12, 2020. Kiongozi wa Taifa alikuwa anatimiza masharti ya Ibara ya 132(1) (b) ya Katiba ya Kenya, kwamba:

“Rais atahutubia Kikao Maalum cha Bunge mara moja kila mwaka na anaweza kuhutubia Bunge wakati wowote mwingine.”

Akizungumza katika hafla hiyo, Spika wa Bunge la Kitaifa, Mhe. Justin Muturi alisema uzinduzi huo sasa ni hatua kubwa katika kuliweka Bunge la Kitaifa la Kenya kwa kiwango sawa na lile la taifa jirani la Tanzania ambalo ndilo la kwanza kukumbatia matumizi ya Kiswahili kuendesha shughuli zake zote.

“Vile vile uvumbuzi huu ni wa kipekee kuwezesha taifa letu la Kenya kudumisha na kuendeleza tamaduni zake kupitia matumizi ya lugha hii inayoeleweka na wananchi wengi,” akasema Bw. Muturi.

Kwa upande wake Katibu wa Bunge la Kitaifa Bw. Michael Sialai, amesema kwamba hatua ya kutafsiri Kanuni za Kudumu za Bunge la Taifa imeingiza Jamhuri ya Kenya katika historia ya kimataifa kama taifa la pili baada ya Canada kuwa na Kanuni katika lugha mbili – Kiingereza na lugha asili za mataifa hayo mawili.

Katibu ameshukuru na kupongeza Jopo aliloteua kutafsiri Kanuni za Bunge la Taifa kutoka Kiingereza hadi Kiswahili. Jopo hilo lilijumuisha Bw. Kipkemoi arap Kirui, Bw. Inzofu Mwale, Bw. Salem Lorot, Bi. Anne Shibuko, Bw. Kalama Mwahunga, Bw. Edwin Mwambeo na Bi. Rabecca Munyao.

Vile vile, Katibu aliwashukuru Maprofesa wa Kiswahili kutoka Vyuo vya Moi, Nairobi na Kenyatta na maafisa kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wao wa kipekee katika kuhariri na kusawazisha tafsiri iliyoandaliwa na Jopo.

Bw. Sialai ambaye ni mweledi wa lugha ya Kiswahili alihutubu kwa lugha ya Kiswahili na kutoa mwongozo mwafaka wa kuigwa na maafisa wake. 

Katika hotuba yake, Rais Kenyatta alisema kuwa matoleo ya Kanuni za Kudumu za Bunge la Taifa katika Kiswahili na Kiingereza-Kiswahili ni ya thamani kubwa maadam yatachangia pakubwa katika kuendeleza tamaduni za nchi hii kupitia kwa lugha ya Kiswahili. 

Rais aliongezea kwamba Bunge la Taifa la Kenya lina tamaduni za kipekee zinazotambulika na kuenziwa na hata kutamaniwa na nchi nyingi za kigeni.

Rais Kenyatta aliwahimiza wabunge kukumbatia lugha ya Kiswahili na kukuza umahiri wa Kiswahili na kujizoesha kutumia Kanuni zilizochapishwa kwa Kiswahili kama ishara ya kuipiga jeki na kukistawisha Kiswahili kama lugha ya taifa na “kuendeleza tamaduni za Kiafrika”. 

“Nawaomba wabunge kuionea fahari lugha ya Kiswahili kwa kuitumia katika mijadala, ukumbini na katika vikao vya kamati” Rais alisisitiza.

Itakumbukwa kwamba katiba ya Kenya inatambua Lugha tatu rasmi za kutumiwa Bungeni ambazo ni; Kiingereza, Kiswahili na Lugha ya Ishara.

 

 

Taarifa ya Deborah Mupusi   na Inzofu Mwale