Skip to main content
Rais Samia Suluhu Hassan Kuzuru Bunge la Kenya

Rais Samia Suluhu Hassan Kuzuru Bunge la Kenya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kutembelea maeneo ya Bunge hivi leo. Baadaye, hapo kesho adhuhuri, Rais huyo ameratibiwa kuhutubia Bunge katika Kikao Maalum. Rais Suluhu anatarajiwa kutoa heshima katika kaburi la Rais wa kwanza wa Kenya, hayati Mzee Jomo Kenyatta. Desturi ya kutoa heshima kwa kaburi hilo la baba muanzilishi imekuwa moja ya shughuli za heshima kuu kwa nchi ya Kenya na imeratibiwa katika Itifaki za Ziara Rasmi za Marais na Wakuu wa Serikali miaka iliyopita. Atakapowasili bungeni kwa shughuli za leo na kesho, Rais Suluhu atapokewa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Mhe. Justin Muturi, na mwenzake wa Seneti, Mhe. Kenneth Lusaka, pamoja na viongozi wengine wa Bunge.

Katika historia ya Bunge la Kenya, Mhe. Rais Samia Suluhu anakuwa Rais wa pili kuhutubia Bunge baada ya mwenzake Rais Jakaya Kikwete kuhutubia Bunge la Kumi na Moja mnamo tarehe 6 Oktoba 2015. Hotuba ya Rais Suluhu ambayo inatarajiwa kwa shauku kubwa ni kwa mujibu wa Kanuni ya 25 ya Bunge la Taifa na ya 26 ya Kanuni za Seneti.

Mabunge ya Tanzania na Kenya yamekuwa na uhusiano mwema kwa miaka nyingi. Ikumbukwe kwamba Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Job Yustino Ndugai, alikuwa mgeni wa heshima katika hafla ya uzinduzi wa Kanuni za Kudumu za Bunge la Taifa la Kenya kwa lugha ya Kiswahili mwaka wa 2019. Vilevile, wafanyakazi wa Bunge la Tanzania—Athman Hussein na Mossy Lukuvi, pamoja na Vidah Mutasa wa BAKITA—walishirikiana kwa karibu sana na wenzao wa Bunge la Kenya katika kutafsiri Kanuni hizo kwa lugha ya Kiswahili.

Ziara hii rasmi ambayo ni ya kwanza tangu Rais Suluhu achukue hatamu za uongozi ni kufuatia mualiko wa Rais Uhuru Kenyatta mwezi uliopita.  Rais Suluhu na mwenyeji wake wanatarajiwa kujadili mbinu za kudumisha na kuimarisha undugu na uchumi kati ya Kenya na jirani wake Tanzania. Wingu la matarajio na mlahaka limetanda nchini tangu jana baada ya ziara yake kutangazwa rasmi. Bungeni, shughuli za mipango ya upokezi zinaendelea huku nchi ikingoja kwa hamu kusikia atakayosema Mhe. Suluhu. Hotuba  yake inakadiriwa kuchukua muda wa saa moja.
 

The website encountered an unexpected error. Please try again later.